WHO yapeleka wataalamu 50 DRC kukabili Ebola

Juhudi za kukabiliana na Ebola katika kituo cha huduma za afya nchini DRC. Picha: WHO

WHO yapeleka wataalamu 50 DRC kukabili Ebola

Afya

Shirika la afya ulimwenguni WHO linapeleka timu ya wataalam 50 wa afya ya jamii nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC ili kusaidia serikali kupambana na mlipuko wa Ebola. Patruck Newman na taarifa kamili

(TAARIFA YA PATRICK NEWMAN)

Kwa mujibu wa shirika hilo wizara ya afya ya DRC tayari imeshaweka mikakati ya dharura ya kudhibiti mlipuko huo na kwa msaada wa WHO na wadau wengine wa kimataifa wanatarajia kuimarisha vituo vya afya katika maeneo ya Bikoro, Iboko na Mbandaka. Tarik Jasarevic ni msemaji wa WHO Geneva

SAUTI YA TARIK JASAREVIC

 “Kuna baadhi ya mambo muhimu ambayo tunatakiwa kuyapa kipaumbele. Kwanza kabisa ni eneo la mapokezi kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa, la pili ni ufuatiliaji wa hali ya wagonjwa, na tatu ni kuwa na uwezo wa maabara ambayo ndiyo tunaishughulikia hivi sasa ili tuwe na uwezo wa kugundua magonjwa . Na mwisho kabisa ni kuwa na timu ya watalamu watakao fanya hizo kazi, muhimu kabisa ni watu ambao wamefundishwa kazi za chanjo.”

(Picha:UNNewsKiswahili/Assumpta Massoi)
Ebola!

Msaada unaotolewa kwa ushirikiano na madaktari wasio na mipaka MSF, shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM na ubia wa chanjo duniani GAVI pia unajumuisha majeneza, vifaa vya kujilinda na maambukizi, usafiri kwa ajili ya kwenda kuzika na kuanzisha usafiri wa anga kwa ajili ya kusafirisha wahudumu na vifaa.

Wizara ya afya ya DRC ilitangaza mlipuko wa Eboka wiki moja iliyopita na hadi sasa kumeripotiwa visa 21 na vifo 17. WHO imetoa dola milioni 1.6 kutoka kwenye mkufo wa dharura wa Umoja wa Mataifa CERF kusaidia kudhibiti mlipuko huo huku wadau wengine wakiwemo USAID, mfuko wa kimataifa wa dharura CFE na serikali ya Italia wakitoa zaidi ya dola milioni 3 , hata hivyo WHO inasema ili kufanikisha udhibti wa mlipuko huo inahitaji jumla ya dola milioni 25 kwa miezi mitatu ijayo.