Waliopoteza maisha kutokana na mafuriko Kenya wafika 132: OCHA
Idadi ya waliokufa kutokana na athari za mafuriko nchini Kenya imepanda. Ofisi ya shirika la Umoja wa Mataifa inayoratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA linasema kuwa hadi sasa idadi ya waliofariki imefikia watu132 huku zaidi ya 311,000 wameachwa bila makazi.
Jens Laerke msemaji wa OCHA, amewaelezea wandishi habari mjini Geneva Uswisi kuhusu hali ilivyo sasa
(SAUTI YA LAERKE)
“Nchini Kenya mvua zinatarajiwa kuendelea kunyesha na kwa mujibu wa idara ya utabiri wa hali ya hewa hadi mwisho wa mwezi huu na kwa hivyo mafuriko mengine yanawezekana kutokea.”
Ameongeza kuwa kazi ya kujiandaa kwa hali ijayo pamoja na kuwashughulikia walioathirika na mafuriko, na kupata manusura inaendelea, ambapo tayari watu 132 wamepoteza maisha wakiweko 30 waliofariki baada ya bwawa moja sehemu za Nakuru kupasuka. Shughuli hizo za uokozi na misaada zinafanywa na serikali ya Kenya kwa ushirikiano na wadau kikiwemo chama cha msalaba mwekundu na shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF.
Na kuhusu nchi jirani za Somalia na Ethiopia amesema
(SAUTI YA LAERKE)
“ Nchini Somalia mvua kali zinaendelea katika mabonde ya mito ya Juba na Shebelle na zinasababisha mito kufurika na kuathiri watu 718,000 wa maeneo hayo huku watu 220,000 wameachwa bila makazi.”