Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nigeria yadhibiti mlipuko wa homa ya Lassa

WHO wakabiliana na homa ya lassa
WHO
WHO wakabiliana na homa ya lassa

Nigeria yadhibiti mlipuko wa homa ya Lassa

Afya

Nchini Nigeria mlipuko wa homa ya Lassa umedhibitiwa baada ya idadi ya visa vya ugonjwa huo kuendelea kupungua ndani y a wiki sita zilizopita.

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limesema hata hivyo lazima wananchi waendelee kuwa makini na kujiepusha na ugonjwa huo ambao huwa unaenea sana nchini humo mara kwa mara.

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika anayehusika na huduma za dharura, Dkt. Ibrahima Socé amesema hadi tarehe 6 mwezi huu, visa vipya vilivyokuwa vimeripotiwa ni vitatu pekee, idadi ambayo ni ndogo sana ikilinganishwa na zama za mlipuko wa homa hiyo.

Amepongeza Nigeria kwa kufikia hatua hiyo muhimu ya kukabili homa ya Lassa akisema sasa ni wakati wa kutumia kile walichojifunza ili kuandaa hatua bora za kujikinga na homa hiyo kwenye nchi zilizo hatarini na ukanda mzima kwa ujumla.

Wakati wa mlipuko wa homa ya Lassa mwaka huu jumla ya vita 423 vilithibitishwa ambapo wagonjwa 106 walifariki dunia wakiwemo wafanyakazi wa huduma za misaada 8.
WHO imesema itaendelea kufuatilia na kusaidia serikali ya Nigeria pamoja nan chi jirani ili kuongeza uwezo wa kujiandaa dhidi ya mlipuko wa Lassa na pia kuchukua hatua sahihi na za haraka pindi mlipuko unapotokea.


Homa ya Lassa husababishwa na virusi na huenezwa kwa binadamu kupitia chakula au vifaa vya nyumbani vyenye mkojo, kinyesi, au damu ya panya. Binadamu anaweza kumwambukiza binadamu mwenzake kupitia majimaji ya  mwilini ya mgonjwa.