Skip to main content

Saa 15 kwa pikipiki kufika eneo lenye Ebola DRC- WHO

Wakati wa mlipuko wa Ebola huko DRC mwaka 2014,  maafisa waandamizi wa UN na serikali ya DRC walitathmini kwa pamoja hatua za kukabiliana na ugonjwa huo.
MONUSCO/Jesus Nzambi
Wakati wa mlipuko wa Ebola huko DRC mwaka 2014, maafisa waandamizi wa UN na serikali ya DRC walitathmini kwa pamoja hatua za kukabiliana na ugonjwa huo.

Saa 15 kwa pikipiki kufika eneo lenye Ebola DRC- WHO

Afya

Kufuatia kuthibitishwa kwa mlipuko wa Ebola huko Equateur nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Umoja wa Mataifa umetangaza fungu la dola milioni 2 kusaidia harakati za kukabiliana na mlipuko huko. 

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA Mark Lowcock amesema fedha hizo zinatoka katika mfumo wa dharura wa umoja huo, CERF.

Tayari watu wawili wamethibitishwa kufariki dunia kutokana na Ebola kati ya visa 32 vilivyoripotiwa hadi jana huko eneo la Bikoro jimbo la Equateur nchini DRC.

OCHA inasema fedha hizo zitasaidia washirika wa kibinadamu kutekeleza hatua  muhimu za kiafya kama vile ufuatiliaji maeneo yenye mlipuko, tiba kwa wagonjwa, kampeni kwa jamii kujikinga na ugonjwa huo pamoja na huduma za mazishi.

Hata hivyo shirika la afya ulimwenguni WHO limesema changamoto ni kufikia eneo hilo kama alivyoeleza Dkt. Peter Salama alipozungumza na waandishi wa habari hii leo huko Geneva, Uswisi.

(Sauti ya Dkt. Peter Salama)

“Kimsingi ni saa 15 kwa pikipiki kutoka mji wa karibu na sasa tunajadiliana na shirika la mpango wa chakula duniani, WFP uwezo wa kufika kwa njia ya anga kwa kuwa tutahitaji msaada wa helikopta na pia tunaangalia jinsi ya kusafisha eneo la njia ya ndege huko Bikoro ili tuweze kufika vizuri.”

CERF iliridhia fungu hilo ndani ya saa 48 tangu kutangaza kwa mlipuko wa Ebola ambapo mlipuko wa mwaka huu ni wa 9 nchini DRC tangu mwaka 1976.