Ndoto zangu za kwenda Ulaya zagonga mwamba

10 Mei 2018

Operesheni ya kuwarejesha nyumbani wakimbizi na wasaka hifadhi waliokuwa kizuizini nchini Libya imeanza tena baada ya kusitishwa kwa miezi miwili.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR limesema katika taarifa yake hii leo kuwa wakimbizi na wasaka hifadhi 132 wamewasili Niger kutoka Libya kwa ndege maalum iliyokodishwa kwa ajili yao.

Miongoni mwao ni mwanamke kutoka Eritrea mwenye umri wa miaka 25 akiwa na mtoto wake.

Amenukuliwa akisema kuwa hatimaye dua zake zimejibiwa na kwamba alitamani kwenda Ulaya  ili mtoto wake aone alichoita mwanga katika nchi anayosema atakuwa salama.

Hata hivyo safari iliishia Libya kwa kuwa mashua aliyopanda ilikuwa na watu wengi na kupinduka karibu na mwambao na hivyo akakamatwa na kuwekwa ndani Libya.

Mjumbe maalum wa UNHCR kwa eneo la Mediteranea ya kati, Vicent Cochetel, amesema kuwa wale walioko vizuizini nchini Libya wako katika hali mbaya na mpango huo ni kujaribu kuokoa wale walio katika hali mbaya zaidi.

Safari hii ya kutoka  Tripoli ndiyo ya  9 tangu operesheni hiyo ianze.

UNHCR inasema idadi kubwa ya wakimbizi na wasaka hifadhi wanazuiliwa katika mazingira magumu sana nchini Libya na kwa muda mrefu.Kwa sasa inakadiria kuwa watu 5,700 ambao wako katika vituo rasmi, kati yao UNHCR inashughulikia 2,637.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud