Burundi mwachieni huru Rukuki- UN

9 Mei 2018

Umoja wa Mataifa umetaka kuachiliwa huru kwa mwanaharakati nchini Burundi ambaye amefungwa gerezani.

Tarehe 3 mwezi uliopita Mahakama Kuu nchini Burundi ilimhukumu Germain Rukuki kifungo cha miaka 32 jela kwa kampeni anazoendesha kupinga mateso kupitia shirika la kiraia la ACAT-Burundi.

Makosa yake yalitajwa kuwa ni pamoja na uasi, kukiuka usalama wa taifa na kumshambulia kiongozi wa nchi.

Kufuatia hukumu hiyo wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa wanataka ifutwe wakisema kuwa ilifanyika kinyume cha taratibu ambapo iliendeshwa kwa kasi isiyo ya kawaida na hakuna ushahidi wowote uliowasilishwa na  upande wa mashtaka dhidi ya mshtakiwa.

Halikadhalika wamesema hukumu ilitolewa wakati wa msako wa watetezi wa haki Burundi na wengi wao walishakumbwa na manyanyaso tangu kulipoibuka harakati baada ya Rais wa sasa Pierre Nkurunzinza kusaka awamu ya tatu ya uongozi.

Wataalamu hao wamesema zaidi ya hayo wana hofu kubwa kuwa hukumu dhidi ya Rukuki ni mfululizo wa hukumu kali za aina hiyo katika miaka iliyotangulia dhidi ya wapaza sauti za haki  hali iliyosababisha wengine kukimbia Burundi.

TAGS: Pierre Nkurunzinza, Germain Rukuki, OHCHR, Burundi,

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud