Iran inatekeleza ahadi zinazohusiana na nyuklia:IAEA

9 Mei 2018

Hadi kufikia sasa shirika la kimataifa la nguvu za atomic IAEA linaweza kuthibitisha kuwa ahadi zinazohusiana na nyuklia zinatekelezwa na Iran.

Kauli hiyo imetolewa leo na mkurugenzi mkuu wa IAEA Yukiya Amano na kuongeza kuwa shirika hilo linafuatilia kwa karibu maendeleo yanayohusiana na mpango wa pamoja wa hatua za kuthibitisha na kufuatilia shughuli za nyuklia za Iran (JCPOA).

 

Amano amesema mchakato unaendelea kama ilivyoombwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa na kuidhinishwa na bodi ya wakurugenzi ya IAEA mwaka 2015.

Jana Jumanne Rais wa Marekani Donald J Trumpalitangaza kujiondoa kwenye mpango wa pamoja wa kudhibiti nyuklia kwa Iran JCPOA na kuanza kuiwekea vikwazo nchi hiyo.

Hali ambayo imeusikitisha Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu antonio Guterres kupitia msemaji wake Stephane Dujarric akasema...

(SAUTI YA STEPHANE DURAJJIC)

Ni muhimu shaka na shuku zote kuhusu utekelezaji wa mpango huo vishughulikiwe kupitia mfumo uliowekwa kwenye JCPOA. Hoja zisizohusiana moja kwa moja na JCPOA zinapaswa kushughulikiwa bila chuki ili kuhifadhi makubaliano hayo na mafanikio yake.”

Amano amesisitiza kuwa IAEA inathibitisha na kufuatilia utekelezaji wa ahadi za nyuklia za Iran kwa mujibu wa mpango huo wa JCPOA.

Iran inakabiliwa na shinikizo kubwa la kimataifa la hakikisho la nia ya shughuli zake za nyuklia chini ya mpango wa JCPOA, ambayo ni faida kubwa ya ukaguzi wa masuala ya nyuklia na upunguzaji wa hatari zake kimataifa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud