Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wapata kiwewe baharini, UNHCR yaelekeza usaidizi

Picha:WFP
Lori la msaada wa kibinadamu likiingia Tripoli, Libya.

Wapata kiwewe baharini, UNHCR yaelekeza usaidizi

Wahamiaji na Wakimbizi

Nchini Libya, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi,  UNHCR limeanza awamu ya pili ya kusaidia wakimbizi na wahamiaji waliookolewa mjini Tripoli baada ya kukabiliwa na hali mbaya baharini.

UNHCR kupitia mtandao wake wa Twitter, inasema wakimbizi na wahamiaji 115 wanapatiwa msaada wa matibabu na ile ya kibinadamu katika kituo cha wanamaji mjini Tripoli.

Watu hao waliterememshwa kutoka kwenye boti baada ya hali zao kuwa mbaya kutokana na ukosefu wa maji mwilini, magonjwa ya ngozi na kiwewe wakati wakiwa safarini kuelekea Ulaya kusaka hali bora.

UNHCR na mdau wake IMC ambao ni kikundi cha kimataifa cha madaktari, wanasema kundi hilo ni la pili, ambapo kundi la kwanza la watu 100 lilipatiwa msaada tarehe 4 mwezi huu wa Mei.

Shirika hilo limetoa wito kwa mipango ya ziada ya uhamiaji na njia za halali za uhamiaji ili kuepusha majanga zaidi kwenye bahari ya Mediteranea.