Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko yawaacha hoi, walala hoi Afrika Mashariki: OCHA

Picha: AU-UN / Tobin Jones
Mtazamo wa angani wa mafuriko karibu na mji wa Jowhar, Somalia.

Mafuriko yawaacha hoi, walala hoi Afrika Mashariki: OCHA

Msaada wa Kibinadamu

Mvua zinazoendelea kunyesha nchini Kenya zimesababisha vifo vya watu takriban 100 na kuwaacha watu 260,000 bila makazi.

Hiyo ni kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA, ambayo imenukuu leo chama cha msalaba mwekundu cha Kenya, KRC.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo msemaji wa OCHA Jens Laerke amesema..

(Sauti ya Jens Laerke)

“Idadi kubwa ya watu waliopoteza makazi yao imeripotiwa kaunti za mto Tana, Turkana, Mandera na Kilifi. Kwa sasa chama hicho cha msalabe mwekundu kina wasiwasi mkubwa kwa  masuala ya kibinadamu, mbali na watu kutokuwa na makazi, ni  kutokea kwa milipuko ya magonjwa sana sana kipindupindu na Chikungunya ugonjwa unaosababishwa na mbu.”

Amesema tayari kipindupindu kimeripotiwa katika kaunti 15 za Kenya tangu mwanzo wa mwaka 2018 ambapo watu 55 kati ya wagonjwa 3,000 wamefariki dunia hadi mwishoni mwa mwezi uliopita.

OCHA imesema kuwa serikali ya Kenya na KRC wanaongoza katika shughuli ya kukabiliana na hali hiyo kwa ushirikiano na mashirika  ya  Umoja wa Mataifa ikiwemo lile la kuhudumia watoto, UNICEF.

PHalikadhalika Bwana Laerke amezungumzia mafuriko kwenye nchi jirani ya Somalia akisema..

(Sauti ya Jens Laerke)

“Mvua kubwa  pamoja na mafuriko katika mabonde ya mito ya  Juba na Shebelle yamesababisha watu 215,000 kuachwa bila makazi. Na kwa ujumla watu walioathirika na mvua hizo nchini Somalia ni 630,000”.

Rais wa Somalia ametangaza hali katika eneo la Belet Weyne kama janga la kitaifa na kuomba msaada kutoka kwa jamii ya kimataifa.

Inakadiriwa kuwa dola za kimarekani millioni 16 ndizo zinahitajika kwa shughuli hiyo huko Somalia.