Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkimbizi afariki dunia baada ya mapigano kambini Kiziba

Wakimbizi wa Rwanda waliokimbilia DRC:Picha na UM/John Isaac

Mkimbizi afariki dunia baada ya mapigano kambini Kiziba

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umetaka mamlaka za Rwanda na wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC waliosaka hifadhi nchini humo wajizuie kufuatia mapigano ya wiki hii yaliyosababisha kifo cha mkimbizi mmoja.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema mpaka sasa mazingira ya mapigano hayo kati ya polisi wa Rwanda na vijana wakimbizi kwenye kambi ya Kiziba hayako bayana lakini linatambua kuwepo kwa mvutano kati ya pande mbili hizo.

UNHCR pamoja na kuelezea masikitiko yake na pia kutuma salamu za rambirambi kwa familia, imesihi pande zote zijizue ili kuepusha shari zaidi ikizingatiwa kuwa tukio la aina hiyo mwezi Februari mwaka huu lilisababisha vifo vya wakimbizi zaidi ya 10.

Andrej Mahecic ni msemaji wa UNHCR, Geneva, Uswisi.

(Sauti ya Andrej Mahecic)

“Mvutano kati ya pande mbili hizo ukiwa ni mkubwa, baadhi ya wakimbizi wamedokeza nia yao ya kutaka kurejea DR Congo, kutokana na kukata tamaa. UNHCR inasihi wakimbizi hao wafanya uamuzi sahihi na si kuchukua uamuzi kwa kuzingatia uvumi.”

Zaidi ya wakimbizi 17,000 wanaishi kwenye kambi hiyo ya Kiziba na wengi wao wamekuwepo kwa zaidi ya miongo miwili.