Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi acheni kushambulia waandishi wa habari

Mkazi wa Pachong huko Sudan Kusini akitoa maoni  yake wakati akihojiwa na mwandishi wa habari wa Radio Miraya ya ujumbe wa  Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS.
UN /Tim McKulka
Mkazi wa Pachong huko Sudan Kusini akitoa maoni yake wakati akihojiwa na mwandishi wa habari wa Radio Miraya ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS.

Viongozi acheni kushambulia waandishi wa habari

Haki za binadamu

Azimio linataka viongozi wa kisiasa na kibiashara waache kuwaona wanahabari kuwa ni maadui bali ni marafiki wanaolenga kufanya jamii iwe bora zaidi.

Kasi ya kutikisa uhuru wa vyombo vya habari na watendaji wake inaongezeka na hivyo kuweka mashakani jukumu lao la kushirikisha umma na kuwajibisha serikali.

Wataalamu wa haki za Umoja wa Mataifa wamesema hayo katika kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani hii leo Mei 3.

Mmoja wao, David Kaye ambaye anahusika na uhuru wa kujieleza amesema waandishi wa habari wanashambuliwa, uhuru wa kujieleza unabinywa na hata watu wanaofanya kazi na serikali huenda mbali zaidi kwa kupeleka matangazo ya biashara kwa vyombo vya habari vinavyounga mkono serikali iliyo madarakani.

Kama hiyo haitoshi, uwasilishaji wa habari wa kidijitali nao wamesema uko mashakani kwa kuwa udhibiti umefikia kiwango cha kubinya uhuru wa kujieleza.

Kwa mantiki hiyo wataalamu hao huru wameunga mkono azimio lililotolewa leo linalopatia msisitizo dhima muhimu ya uhuru wa vyombo vya habari katika jamii za kidemokrasia na kuelezea hofu juu ya mashambulizi dhidi ya wanahabari.

Wamesema vyombo huru vya habari na vinavyojitegemea vinafanikisha demokrasia na uwajibikaji ilihali mashambulizi dhidi ya wanahabari na tasnia ya habari hukandamiza hoja ya ushiriki wa umma na uwajibishaji wa serikali.

Wametaka serikali zichukue hatua kuzuia vitendo hivyo vikisema vinazidi kushamiri kutokana na wanahabari kuonekana kuwa ni maadui wa viongozi wa kisiasa na kibiashara ilhali wanafanya kazi yao ya uchunguzi kwa maslahi ya umma.