Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahudumu 10 wa misaada waachiliwa bila hata kovu Sudan Kusini

Picha: UNHCR/Jiro Ose
Misaada kwa wakimbizi wa Sudan Kusini Ikisafirishwa na wahudumu wa misaada ya kibinadamu.

Wahudumu 10 wa misaada waachiliwa bila hata kovu Sudan Kusini

Amani na Usalama

Wafanyakazi 10 wa misaada ya kibinadamu waliokuwa wanashikiliwa mateka na kundi lenye silaha tangu Jumatano iliyopita , Aprili 25, nje kidogo ya mji wa Yei nchini Sudan, kusini leo wameaachiliwa huru.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF wafanyakazi hao wamerejea Juba salama, na baada ya kufanyiwa uchunguzi na madaktari wameelezwa kuwa buheri wa afya.

Henrietta H. Fore mkurugenzi mtendaji wa UNICEF  kwa furaha ya kuachiliwa kwao amesema “ni habari njema kwa wafanyakazi wenzetu kurejea , tunamshukuru kila mmoja aliyesaidia kuachiliwa kwao, na tunatoa wito tena kwa pande zote kwenye mzozo huu kutowalenga au kuwazuia wafanyakazi wa misaada kutimiza wajibu wao unaookoa maisha , na matukio kama haya ni lazima yakome.”

Wahudumu hao wa misaada wakiwemo wafanyakazi wawili wa UNICEF walitoweka walipokuwa wakisafiri kwa gari kutoka Yei kwenda Tore ambako ilikuwa waende kutathimini mahitaji ya kibinadamu.

Wafanyakazi hao punde wataungana na familia zao na watapatiwa msaada wa kisaikolojia na usahuri nasaha.