Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya wasaka hifadhi Sudan Kusini yaongezeka - UNMISS

Picha: UNMISS / Isaac Billy
Askari wa kulinda amani UNMISS katika kituo cha ulinzi wa raia cha Bentiu.

Idadi ya wasaka hifadhi Sudan Kusini yaongezeka - UNMISS

Amani na Usalama

Idadi ya wakimbizi wa ndani wanaosaka hifadhi kwenye vituo sita vya ulinzi wa raia nchini Sudan Kusini vilivyo chini ya ujumbe wa wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, inazidi kuongezeka.

Katika taarifa yake ya mwisho wa mwezi iliyotolewa leo, UNMISS inasema ongezeko hilo linatokana na kuzuka tena  kwa vita hivi karibuni katika baadhi ya majimbo nchini humo.

Idadi ya wakimbizi walio kwenye vituo hivyo sasa ni zaidi ya laki mbili ambapo huko Bentiu jimbo la Unity ni zaidi ya laki moja, Malakal jimbo la Upper Nile ni zaidi ya elfu ishirini na wanne, na huko Equitoria ya Kati ikiwemo mjini Juba ni zaidi ya elfu thelathini.

Majimbo mengine ni pamoja na Jonglei na huko Bahl el Ghazal magharibi .

UNMISS pamoja na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa wanaendelea na juhudi za ulinzi wa amani nchini Sudan Kusini na pia usaidizi wa kibinadamu  kwa waathirika wakuu katika migogoro hii ambao ni wanawake , wazee na watoto.