Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watawa Ufaransa wafungua milango yao kwa wakimbizi

Mkimbizi mwanamke kutoka Eritrea akiwa na rafiki wake katika basi ya kusafiririsha wakimbizi kutoka Libya kuelekea Ulaya.
UNHCR/Alessandro Penso
Mkimbizi mwanamke kutoka Eritrea akiwa na rafiki wake katika basi ya kusafiririsha wakimbizi kutoka Libya kuelekea Ulaya.

Watawa Ufaransa wafungua milango yao kwa wakimbizi

Wahamiaji na Wakimbizi

Baada ya kupitia machungu na mateso makali korokoroni nchini Libya hatimaye wakimbizi 56 kutoka mataifa mbalimbali wamepewa hifadhi ya kudumu kwenye makazi ya watawa wa kikatoliki wa shirika la wafransisca  kaskazini mashariki  mwa Ufaransa.

Wakimbizi hao ambao wengi wao ni wanawake na watoto kutoka Ethiopia, Eritrea, Afrika ya kati na Sudan walisafirihswa kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, kupitia mpango wake wakuwatafutia makazi ya kudumu wakimbizi katika nchi ya tatu.

Miongoni mwao ni Mohammed, mkimbizi kutoka Eritrea pamoja na  mke wake na watoto wanne ambaye baada ya  kupitia mateso Libya, hakuficha hisia zake kuhusu mustakhabali wa familia yake kwa sasa.

(Sauti ya Mohammed)

"Ikimpendeza Mungu maisha yetu yatakuwa mazuri , ninaamini hivyo. Nina matumaini  kwangu na kwa wengine pia. Mungu akipenda natumai elimu ya watoto wetu itakuwa bora hapa. Natamani nipate kazi,  itakuwa jambo jema."

France Horizon limechukua jukumu la kuwasaidia wakimbizi hao katika masuala mbalimbali kama  ushauri nasaha kwa waliopitia zahma mbalimbali nchini Libya na pia msuala ya utamaduni, lugha na hatua za kuanza upya maisha katika nchi hiyo.

Hattice Calik ni mratibu wa shirika hilo.

(Sauti ya Haticce Calik)

"Sasa wametujua , wameshaanza kutozoea, ile hali ya hapo awali ya uwoga imekwisha . Inatia moyo sana kuona kwamba hatimaye watu hawa wako katika mazingira yalio salama ."

Majirani na wakazi wa kijiji hicho pia wameonyesha nia ya kuwapokea wakimbizi hao kwa kuwakaribisha watoto wao katika shule zao bila kuwabagua na kuwafundisha tamaduni  na pia lugha ya kifaransa.

Wakimbizi hao watakaa katika makazi ya watawa kwa miezi 4 na baadaye wakishapata ajira wataanza taratibu za kutafuta sehemu yao ya kuishi.