Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumieni mkutano wenu kuleta upatanishi -Guterres awaeleza viongozi wa Korea

Rais Moon jae-in(kulia) wa Korea Kusini akiwa na Mwenyekiti wa  tume ya masuala ya taifa ya Korea Kaskazini wakiwa Panmunjeom.
Picha ya kikosi cha habari cha Mkutano wa nchi mbili wa Korea mbili.
Rais Moon jae-in(kulia) wa Korea Kusini akiwa na Mwenyekiti wa tume ya masuala ya taifa ya Korea Kaskazini wakiwa Panmunjeom.

Tumieni mkutano wenu kuleta upatanishi -Guterres awaeleza viongozi wa Korea

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha hatua ya leo ya mkutano kati ya viongozi wa Korea Kaskazini na Korea Kusini akisema ni ya kihistoria.

Bwana Guterres kupitia taarifa ya msemaji wake ameeleza kuwa yuko tayari kusaidia Korea mbili katika mchakato wao mpya wa kuona zinapatana.

Utayari wa Katibu Mkuu umo katika ujumbe ambao ameutoa baada ya kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un kukutana ana kwa ana na Rais wa Korea Kusini Moon Jae hii leo.

Viongozi hao wawili wamekutana Korea Kusini ambapo wameahidi kutangaza kukomesha mwaka huu kile walichokiita mvutano baina ya Korea mbili . Pia viongozi hao katika mazungumzo yao wameahidii kuondoa silaha za nyuklia kwenye rasi ya Korea.

Ni kufuatia kauli hizo ambapo Bwana Guterres amesema amefurahia mkutano huo na kuuita wa kihistoria, akisifu ujasiri wa viongozi hao. 

Taarifa ya msemaji wa Guterres imeeleza kuwa watu wengi duniani wamefurahishwa na picha zinazoonyesha viongozi hao wawili wa Korea Kaskazini na Korea Kusini wakikutana kwa lengo la kuleta amani katika rasi ya Korea.

Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amewapongeza viongozi wote waliofanikisha mkutano huo na vilevile  amewaomba viongozi husika  kutumia mkutano huu kuweza kuleta upatanishi.

Amesema ana matumaini kuwa mkutano mwingine wa ngazi ya juu kati ya viongozi wa Korea Kaskazini na Marekani unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni utaimarisha yale yaliyofikiwa katika mkutano kati ya viongozi wa Korea mbili.