Ugiriki boresha mazingira kwa wakimbizi Evros

27 Aprili 2018

Umoja wa Mataifa umeisihi Ugiriki iboreshe mazingira na kasi ya mapokezi ya wasaka hifadhi kwenye mkoa wa Evros ambako wakimbizi wanazidi kumiminika wakipitia mpaka wa nchi hiyo na Uturuki.

Yaelezwa kuwa mwezi huu pekee watu 2,900 wameingia Evros wengi wao wakiwa ni wanafamilia kutoka Syria na Iraq, idadi ambayo inaelezwa ni nusu ya watu wote walioingia eneo hilo mwaka jana.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linasema mamia ya watu wanashikiliwa polisi huku watu wanane wakiripotiwa kufariki dunia tangu kuanza mwaka huu wakijaribu kuvuka mto Evros kuingia Ugiriki.

Kama hiyo haitoshi, watu hao wamejazana kwenye kituo cha mapokezi wengine wakilala kwenye sakafu kwa kuwa kituo hicho kinaweza kuhudumia watu 240 tu na sasa idadi imezidi uwezo.

Charlie Yaxley  ni msemaji wa UNHCR Geneva, Uswisi na anasema kwamba Mamia ya watu wanaoshikiliwa kwenye mazingira hayo duni ni pamoja na wajawazito, watoto wadogo na watu wanaohitaji matibabu na ushauri wa kisaikolojia.

Amesema ingawa wanakaribisha hatua ya karibuni ya kuachiliwa kutoka korokoroni kwa zaidi ya watu 2,500..

(sauti ya Charlie Yaxlye)

“ UNHCR inapendekeza kuboreshwa kwa mazingira ya kituo cha mapokezi na kupanua uwezo wake.”

Amesema UNHCR itaendelea kushirikiana na mamlaka za Ugiriki kwa kuwapatia misaada ya kiufundi na vifaa ikiwemo vile vya malazi na kujisafi kwa ajili ya wasaka hifadhi hao.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter