Bila ufadhili mpya roho mkononi kwa maelfu ya Warohingya huko Bangladesh:IOM

27 Aprili 2018

Juhudi za mashirika ya umoja wa Mataifa za kunusuru maisha ya maelfu ya Warohingya waliokimbilia Bangladesh dhidi ya msimu wa pepo kali na mvua za monsoon zinazotarajiwa kuanza mapema mwezi ujao , zitagonga mwamba endapo hakutapatika ufadhili mpya haraka.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM katika wiki sita zijazo ni lazima ufadhili mpya upatikane la sivyo maisha ya maelfu ya wakimbizi wa Rohingya yatakuwa katika hatari kubwa ya athari za mafuriko, mapotromoko na uharibifu mwingine utakaosababishwa na msimu wa monsoon. Joel Milliman ni msemaji wa IOM Geneva

(SAUTI YA JOEL MILLIMAN)

“Bila msaada wengi itabidi wasalie katika maeneo ya hatari na wengine maelfu watakuwa katika hatari endapo barabara hazitopitika na msaada muhimu wa chakula na huduma za afya hazitoweza kuwafikia, na familia zilizo hatarini hazitopata makazi mapya wala kukarabitiwa nyumba zao zilizoathirikwa wakati wa kimbunga. Msfumo wa maji safi unaweza kusambaratika na kuwaweka maelfu ya wakaimbizi katika hatari ya maradhi yatokanayo na maji .”

Ameongeza kuwa ingawa baadhi ya wakimbizi wameshahamishwa na wengine kwenda katika nchi jirani kama Indonesia lakini bado idadi kubwa wako katika kambi hizo.

Takriban wakimbizi milioni moja wa Rohingya hivi sasa wanaishi kwenye makambi Cox’s Bazar nchini Bangladesh baada ya kukimbia machafuko nchini Myanmar tangu Agosti mwaka jana, na kati yao 120, 000 wameelezwa kuwa katika hatari ya mafuriko na maporomoko ya udongo huku wengine 25,000 wakiwa katika hatari kubwa zaidi ya maporomoko kutokana na eneo zilipo kambi wanazoishi.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter