Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wafanyakazi 10 watoweka nchini Sudan Kusini.

Watoa misaada wa chama cha mwezi mwekundu. Wenzao kama hao 10 wametoweka Sudan Kusini.
Picha ya chama cha mwezi mwekundu cha Syria
Watoa misaada wa chama cha mwezi mwekundu. Wenzao kama hao 10 wametoweka Sudan Kusini.

Wafanyakazi 10 watoweka nchini Sudan Kusini.

Amani na Usalama

Wafanyakazi 10 wa kutoa misaada ya kibinadamu nchini Sudan Kusini wametoweka wakati wakiwa kwenye msafara wa kutathmini mahitaji ya kibinadammu huko Yei jimbo la Equatoria ya Kati nchini humo.

Mratibu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini humo Alain Noudehou amesema wafanyakazi hao walipotea jana Jumatano na hadi sasa hawafamiki waliko.

Bwana Noudehou amesema wafanyakazi wote ni raia wa Sudan Kusini na amesihi waachiliwe mara moja bila masharti yoyote.

Huku akielezea kuwa wana hofu kubwa kuhusu huko waliko wafanyakazi hao, Bwana Noudehou amekumbusha kuwa wafanyakazi hao pamoja na Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia wako nchini Sudan Kusini kwa ajili ya kusadia na hivyo hawapaswi kulengwa.

Mratibu huyo wa misaada ya kibinamu amesihi pande hasimu nchini Sudan Kusini kuhakikisha kuna usalama ili watoa misaada waweze kufanya kazi yao bila hofu.

Tukio hili la kutoweka kwa wafanyakazi wa misaada nchini Sudan Kusini ni la pili mwezi huu wa Aprili pekee na ni la tatu ndani ya kipindi cha miezi sita.