Wachunguzi wa OPCW wachukua sampuli Douma

25 Aprili 2018

Hatimaye wachunguzi kutoka shirika la kuzuia silaha za kemikali, OPCW wameweza kufika eneo la pili huko Douma nchini Syria kunakodaiwa kutumika silaha za kemikali wakati wa shambulio tarehe 7 mwezi huu wa Aprili.

Taarifa OPCW iliyotolewa The Hague, Uholanzi hii leo imesema kikosi cha wachunguzi hao,  au FFM, kimechukua sampuli za udongo wa eneo hilo ambapo zitajumuishwa na sampuli nyingine katika maabara ya shirika hilo huko Rijswik Uholanzi. 
 
Baadae sampuli hizo zitagawanywa  makundi kadhaa na kutumwa katika maabara zingine za OPCW kwa uchunguzi zaidi.
 
Wachunguzi hao walikuwa waingie eneo hilo tarehe 8 punde tu baada ya mashambulizi lakini kutokana na hali ya usalama  kutokuwa nzuri, waliweze kufika Douma tarehe 21 mwezi huu na leo wameweza kuingia eneo la pili.
 
Wachunguzi hao wanapatiwa ulinzi mkali kutoka  idara ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya usalama-UNDSS kwa ushirikiano na  wakuu wa Syria pamoja na polisi ya jeshi la Urusi.
 
Tayari wameweza kuhoji baadhi ya wale wanaohusika na tukio la Douma ambao walipelekwa mjini Damascus.
 
URUSI KUPELEKA MASHAHIDI WA DOUMA MBELE YA OPCW
 
Na hayo yakiarifiwa , makao makuu ya OPCW yanaripoti kuwa ujumbe wq Urusi kwenye shirika hilo, unapanga kuwasilisha maelezo yake mbele ya nchi wanachama wa shirika hilo mjini The Hague kesho Aprili 26. 
 
Ujumbe huo utapeleka baadhi ya raia wa Syria ili kutoa ushahidi juu ya tukio la Douma.
 
Hatua hiyo ya Urusi inafuatia ombi la OPCW la kutaka mataifa husika kubadilishana taarifa. 
 
Hata hivyo OPCW imeshauri ni vema mashahidi hao wahojiwe kwanza na kikosi cha uchunguzi au FFM, na kupendekeza kuwa mkutano kama ule unaopendekezwa na Urusi ufanywe baada ya  uchunguzi wa FFM.
 
 Hata hivyo Urusi kwa upande wake inasema itaendelea na  mipango yake na kuongeza kuwa haina nia ya kuingilia kati kazi za FFM.
 

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter