Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwekeza kwa afya ya Wasyria ni kuwekeza katika mustakhbali wao: WHO

Moja ya kliniki sita za kuhamahama zinazotolewa na WHO kutoa huduma za afya kwa watu wanaokimbia ukatili huko Aleppo, Syria. Picha: WHO Syria

Kuwekeza kwa afya ya Wasyria ni kuwekeza katika mustakhbali wao: WHO

Msaada wa Kibinadamu

Wakati jumuiya ya kimataifa ikikusanyika mjini Brussels Ubelgiji ili kuonyesha mshikamano na watu wa Syria na kusaka suluhu ya kisiasa ya vita nchini humo, shirika la afya ulimwenguni WHO, limetoa wito wa kuwekeza katika afya kunusuru maisha ya mamilioni ya watu nchini humo.

Shirika hilo linasema uwekezaji katika afya utalinda maisha ya watu milioni 17 wanaume, wanawake na watoto walio katika hali tete ndani ya Syria na  nchi tano za jirani.

Limeongeza kuwa kila siku Wasyria wanafariki dunia kwa magonjwa yanayotibika kirahisi. Ndani ya nchi upungufu mkubwa wa vifaa vya tiba, kutokuwepo usalama na kuvurugika kwa mfumo wa afya kumesababisha mamilioni ya watu kuhitaji msaada wa huduma za afya.

Wakati huohuo Wasyria waliokimbilia nchi jirani wamejikuta wako njia panda, idadi kubwa wakiishi chini ya mstari wa umasikini na kushindwa kumudu huduma za afya na vita vinavyoendelea vinazidi kuyaweka rehani maisha yao.

Tangu kuanza kwa mgogoro watu milioni 11.3 ndani ya Syria wanahitaji msaada wa huduma za afya, wakati huu chini ya nusu ya vituo vya afya ndio vinavyofanya kazi huku vikikabiliwa na changamoto nyingi.

Kwenye mkutano huo mjini Brussels WHO inasisitiza kwamba afya ni haki ya binadamu ambayo ni lazima iheshimiwe na pande zote katika mzozo wa Syria na mashambulizi dhidi ya wahudumu na vituo vya afya ni lazima yakome.

WHO na wadau wa afya wanahitaji dola milioni 426.4 ili kuwafikia Wasyria milioni 11.3 mwaka huu 2018 kwa huduma muhimu za afya wanazohitaji.