Machungu niliyopitia Libya hayafikiriki

Wahamiaji warejea nyumbani kwa hiari. Picha: IOM

Machungu niliyopitia Libya hayafikiriki

Wahamiaji na Wakimbizi

Nimepitia machungu makubwa zaidi nchini Libya sasa nimerejea nyumbani nina imani kubwa. Hiyo ni kauli ya mmoja wa raia 121 wa Cameroon ambao wamerejeshwa nyumbani hivi karibuni kutoka Libya baada ya ndoto zao za kuelekea Ulaya kusaka maisha bora kutumbukia nyongo.

Ingawa hakupatiwa jina, raia huyo wa Cameroon akingumza baada ya ndege yao kutua kwenye uwanja wa ndege wa Nsimalen mjini Yaoundé amesema akiwa Libya alihamishwa kutoka gereza moja hadi jingine na sasa anajuta na kushangaa ni jambo gani lilimsukuma kukimbia nchi yake.

Mkuu wa shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM,  nchini Cameroon, Boubacar Seybou amesema ndege iliyowarejesha nyumbani ilifanikishwa kwa ushirikiano kati ya IOM na Muungano wa Ulaya, EU.

Hadi sasa raia 1,357 wa CAmeroon wakiwemo wanawake 252 wamerejeshwa nyumbani kwa hiari chini  ya mpango huo ambapo wanapatiwa usaidizi wa kuwawezesha kujikwamua kimaisha.