Tusichoke kuwekeza katka elimu ya watoto Syria: Cappelaere.

Ripoti ya hivi karibuni ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani UNICEF, imebaini kuwa licha ya vita vya zaidi ya miaka 7 nchini Syria, watoto milioni 4.9 wameendelea kupata elimu, japo katika mazingira magumu .
Geert Cappelaere. ambaye ni mkurugenzi wa UNICEF ukanda wa Mashariki ya kati na kaskazini mwa Afrika amesema, misaada kutoka kwa wahisani na kazi nzuri ya kujitolea inayofanywa na waalimu nchini humo ndio sababu kuu ya kufikia mafanikio hayo ya elimu kwa watoto.
Aidha ripoti imesema zaidi ya asilimia 90 ya watoto ambao wanapata elimu katika shule za umma wapo Syria na wengine ni wakimbizi wa Syria walioko Lebanon na Jordan ambao wanaendelea kupata elimu katika shule za umma za nchi hizo.
Kwa mujibu wa UNICEF japo wamefanikiwa kwa kiasi, mgogoro wa Syria ambao umedumu kwa zaidi ya miaka saba umewakosesha elimu zaidi ya watoto milioni 2.8, ambapo tangu mwaka 2011 shule Zaidi ya 309 zimeharibiwa.
Ripoti imeongeza kuwa shule moja kati ya 3 zimesambaratishwa kabisa na kusababisha zaidi ya asilimia 40 ya watoto wenye umri kati ya miaka 15 na 17 kutokuwa shuleni na kuishia kwenyemakundi ya kigaidi baada ya kurubuniwa na wahalifu.