Hatua ya DPRK ni ya kuungwa mkono

23 Aprili 2018

Vitisho vya matumizi ya nyuklia kwa makusudi au vinginevyo vinaongezeka hivi sasa na kuleta changamoto kama ilivyokuwa miaka 50 iliyopita wakati mkataba wa kudhibiti kuenea kwa silaha duniani, NPT ulipopitishwa.

Mwakilishi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kudhibiti matumizi ya silaha, Izumi Nakamitsu amesema hayo leo mjini Geneva, Uswisi mwanzoni mwa kikao cha mapitio ya awali ya mkataba huo.

Amesema vitisho hivyo vitaendelea kuwepo iwapo mataifa yataendelea kuhifadhi silaha hizo akitolea mfano maeneo ya rasi ya Korea.

Hata hivyo amekaribisha tamko la hivi karibuni la Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK ya kusitisha majaribio na matumizi ya nyuklia akisema..

(Sauti ya Izumi Nakamitsu)

“Uamuzi wa DPRK wa kusitisha majaribio ya urushaji wa makombora ya masafa marefu na kuharibu eneo lake la majaribio ya silaha za nyuklia, ni hatua inayokaribishwa ambayo tunatumai itachangia katika kujenga imani na kuendeleza mazingira ya mazungumzo na mashauriano ya dhati.”

Kikao hicho kitakachomalizika tarehe 4 mwezi ujao ni cha pili kati ya vitatu vinavyotakiwa kuandaa ajenda za mapitio ya mkataba huo wa NPT kwa mwaka 2020.

Kwa mantiki hiyo Bi. Nakamitsu amesihi wajumbe kuwa na mjadala wa kina kuhakikisha matokeo ya kikao hicho yataboresha mkataba huo wa kudhibiti kuenea kwa silaha duniani. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter