Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usalama mpakani mwa Ecuador na Colombia vyatutia hofu- UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres. Picha: UM

Usalama mpakani mwa Ecuador na Colombia vyatutia hofu- UN

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake juu ya kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama mpakani mwa Ecuador na Colombia.

Kauli hiyo inafuatia kitendo cha hivi karibuni cha kutekwa nyara na hatimaye kuuawa kwa wafanyakazi watatu wa vyombo va habari huko Ecuador sambamba na kutekwa kwa raia wawili wengine wa Ecuador.

Yaripotiwa kuwa watu hao ambao ni waandishi wa habari wawili na dereva mmoja walitekwa nyara tarehe 26 mwezi uliopita na hatimaye kuthibitishwa kuwa wameuawa tarehe 13 mwezi huu kwenye eneo hilo la mpakani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia taarifa ya msemaji wake ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga wa tukio hilo na kuelezea mshikamano wake na serikali na wananchi wa Ecuador.

MAKUNDI YA UHALIFU MPAKANI YANATISHIA USALAMA

Guterres amesema vitendo hivyo vinaonyesha vitisho vitokavyo kwa makundi ya kihalifu yaliyopo mpakani mwa Ecuador na Colombia na kwa kuzingatia hilo amekaribisha ushirikiano wa karibu kati ya nchi hizo ili kushughulikia kitisho hicho.

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia serikali hizo kwenye maeneo ambayo itaonekana ni lazima kufanya hivyo.