Misaada yafikia wakimbizi wa ndani kusini mwa Libya

Image

Misaada yafikia wakimbizi wa ndani kusini mwa Libya

Msaada wa Kibinadamu

Hatimaye misafara iliyosheheni misaada ya kibinadamu imewafikia wakimbizi wa ndani nchini Libya waliopo mji wa Marzuk kusini mwa nchi hiyo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linasema wakimbizi hao ni manusura wa mapigano ya hivi karibuni kati ya vikundi vilivyojihami kwenye mji wa Sabha, ulioko takribani kilimeta 760, kusini mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Msemaji wa UNHCR mjini Geneva Uswisi, Andrej Mahecic amesema mapigano hayo yalisambaratisha familia 1900 ambako walikokimbilia kwenye mji wa Sabha usalama haukuwa wa kutosha kwa misaada kuweza kuwafikia.

Amesema tarehe 5 mwezi huu waliweza kufikisha misaada kama vile blanketi, magodoro, vifaa vya kujisafi na kupikia kwa familia 850 lakini baadaye hali ya usalama haikuwa nzuri na hivyo walisitisha mgao.

(Sauti ya Andrej Mahecic)

“Hata hivyo, mapema wiki hii, jamii kwenye maeneo hayo zilianza kutumia barabara kuu kutoka Sabha kwenda Murzuk. Hii ilipatia fursa UNHCR kusambasa haraka misaada muhimu huko Murzuk amako siku ya Jumatano familia 370 zilipata misaada inayohitaji.”

Nchini Libya hivi sasa zaidi ya wakimbizi wa ndani 184,000 wanahitaji misaada ya kibinadamu bila kusahau wengine 368,000 waliorejea makwao lakini bado hawawezi kukimu Maisha yao.