Tunisia yapiga hatua katika masuala ya haki za binadamu : Shaheed

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imeipongeza Tunisia kwa kupiga hatua katika mchakato wa kidemokrasia ikiwemo utekelezaji wa haki za kibinadamu baada ya wimbi la mapinduzi lililozikumba baadhi ya nchi za kaskazini mwa Afrika miaka 7 iliyopita.
Baada ya ziara yake ya kikazi nchini Tunisia Bw. Ahmed Shaheed ambaye ni mtaalam huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema Tunisia imepiga hatua katika utekelezaji wa mchakato wa kidemokrasia japo bado kuna changamoto katika mfumo wa mahakama ambao baadhi ya vifungu haviendani na kanuni za haki za binadamu ,akiongeza ufinyu wa uhuru wa kuabudu ambayo ni moja ya changamoto inayotakiwa kufanyiwa kazi.
Aidha mtalaam huyo katika ripoti yake amesema Tunisia inakabiliwa pia na changamoto zingine ikiwa ni pamoja na vitendo vya kigaidi , kuhakikishia jamii maendeleo endelevu ya kiuchumi, kuimarisha taasisi za kidemokrasia, utawala wa sheria, na kubadilisha mitazamo ya kiitikadi kwa baadhi ya jamii .
Katika ziara yake huko Tunisia Bwana Shaheed alikutana na vyongozi wa serikali akiwemo Waziri Mkuu, viongozi wa dini na viongozi wa asasi mbalimbali za kiraia.
Ripoti hiyo itawasilishwa katika Baraza la haki za kibinadamu machi mwakani.