Maeneo mapya ya urithi wa kilimo yatajwa na FAO
Maeneo mapya 13 ya urithi wa kilimo yametajwa na shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO na kutambuliwa rasmi kama mifumo ya urithi wa kilimo muhimu duniani-GIAHS.
Katika sherehe iliofanyika leo mjini Roma nchini Italia, maeneo husika ni pamoja na yale ya kilimo cha mpunga milimani pamoja na kilimo cha wasabi kwenye makasha huko Japan.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO Bi Maria Helena Semedo akizungumza kwenye hafla hiyo amegusia umuhimu wa mifumo hii ya urithi wa kilimo endelevu.
(Sautiya Maria Semedo)
“Inahifadhi bayonuwai pamoja na kuendeleza huduma mbalimbali , uwepo wa chakula pamoja na kulinda maisha”
Ameongeza kuwa mifumo hiyo inaashiria uwiano mwema baina ya binadamu na mazingira.
Bi. Semedo amesema umuhimu wa wa urithi wa maeneo ya kilimo unajumuisha maeneo ya mifumo ya ekolojia ambapo matumizi ya maji,uhai wa ardhi pamoja na mifumo mingine inaunganishwa pamoja na sheria za ardhi.
Halikadhalika mifumo ya urithi inaleta pamoja uchumi, mazingira , jamii na utamaduni ambavyo ni nguzo za malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.
Kutajwa kwa maeneo hayo mapya 13 kunafanya idadi ya maeneo ya urithi wa mifumo ya kilimo duniani kufikia 50.
Nchi zingine ambazo zimejumuika kwenye maeneo hayo ya urithi ya mifumo ya kilimo ni Japan,Mexico, Ureno, Misri na Sri Lanka.