Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mbu wa Zika na Malaria wapata kiboko yao

Mbu wa Aedes anayeambukiza virusi vya Zika. Picha ya WHO

Mbu wa Zika na Malaria wapata kiboko yao

Afya

Hatimaye ndege zisizo na rubani au drones zimetumika kuachia kutoka angani mbu dume tasa kama njia mojawapo ya kudhibiti maambukizi ya ugonjwa hatari wa Zika na mengineyo.

Majaribio hayo  yalifanyika mwezi uliopita huko Brazil ambapo mbu hao aina ya Aedes walifanywa tasa kwa kutumia mionzi na imeelezwa kuwa majaribio hayo yalikuwa na mafanikio makubwa.

Shirika la nishati ya atomiki la Umoja wa Mataifa, IAEA limesema baada ya kupigwa mionzi hiyo mbu dume huwa tasa na hivyo hata wanapokutana na mbu jike hawawezi kuzaliana na hivyo kupunguza na hatimaye kutokomeza wadudu hao.

Jeremy Bouyer, kutoka mradi wa pamoja wa FAO na IAEA amesema mbinu hiyo ya kutumia ndege zisizo na rubani imekuwa muarobaini mkubwa kwa kuwa walikuwa wanakabiliwa na kikwazo kikubwa cha jinsi ya kuachia mbu hao tasa kutoka angani.

Mbinu hiyo inahitaji uachiaji wa mbu hao aina ya Aedes waachiliwe kwa kiwango kikubwa katika mazingira bora na imekuwa vigumu kuwasambaza kwa kutumia ndege kwa kuwa wanakuwa wamekufa iwapo watakwenda umbali mrefu angani kutoka usawa wa bahari.