Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtoto hapaswi kubeba bunduki na kupigana-UNICEF

Askari watoto nchini Sudan Kusini wakabidhiwa kwa UNICEF
UNICEF Sudan Kusini/Marinetta Peru
Askari watoto nchini Sudan Kusini wakabidhiwa kwa UNICEF

Mtoto hapaswi kubeba bunduki na kupigana-UNICEF

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Zaidi ya watoto 200 wameachiliwa huru na makundi yenye silaha nchini Sudan Kusini na idadi hiyo imefanya watoto walioachiliwa huru na makundi hayo tangu mwanzo wa mwaka huu 2018 ifikie 500. 

Zaidi ya watoto 200 wameachiliwa huru na makundi yenye silaha nchini Sudan Kusini na idadi hiyo imefanya watoto walioachiliwa huru na makundi hayo tangu mwanzo wa mwaka huu 2018 ifikie 500. Siraj Kalyango na ripoti kamili.

(Taarifa ya Siraj Kalyango)

Hii ni awamu ya pili ya watoto kuachiliwa huru katika mpango unaodhaminiwa na shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa mataifa la UNICEF.

Kufuatia hatua hiyo, mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan Kusini, Mahimbo Mdoe, amesema hakuna mtoto anayepaswa kubeba bunduki na kupigana.

Amesema kila mtoto anayeachiliwa huru, siku hiyo huwa ndio mwanzo wa maisha  yake mapya na kukariri kuwa UNICEF inajivunia  kuwasaidia watoto hao warejee katika familia zao na kuanza maisha mapya.

Wakati wa sherehe ya kuachiliwa rasmi,mjini Yambiyo watoto hao walipokonywa silaha na kupatiwa nguo za kiraia na baadaye watapatiwa ushauri nasaha kama sehemu ya kuwajumuisha katika maisha mapya, mpango ambao unatekelezwa na UNICEF.

Miongoni mwa watoto hao waliochiliwa huru, 112 ni wavulana ilhali wasichana ni 95.

Wote walitoka katika makundi mawili ya  Sudan National Liberation Movement, -SSNLM- ambalo lilisaini mktaba wa mani na serikali mwaka 2016 pamoja na lile la Sudan People’s Liberation Army-upande wa upinzani, SPLA-IO.

UNICEF inasema  watoto wengine takriban 1,000 wataachiliwa huru miezi michache ijayo.