Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwapa kipaumbele Wayemen ndio suluhu pekee ya amani nchini humo:

Familia nchini Yemen wapata lishe muhimu mara moja tu kwa siku. Picha: WFP

Kuwapa kipaumbele Wayemen ndio suluhu pekee ya amani nchini humo:

Amani na Usalama

Kuwasikiliza na kuwashirikisha Wayemen katika mgogoro unaowahusu ni jambo la muhimu sana kwani suluhu ya vita nchini Yemen inaweza kutoka miongoni mwao na hasa kwa viongozi wao kuweka tofauti zao kando na kuafikiana sio kwa njia ya vita bali kupitia majadiliano.

Hayo yamesemwa na Martin Griffiths mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Yemen, katika mjadala uliofanyika leo kwenye baraza la usalama mjini New york kujadili hali na hatua zilizopigwa nchini humo.

Amesisitiza kuwa kuwapa kipaumbele Wayemen sio tu ni haki bali ndio njia pekee itakayofanikisha  na kurejesha amani nchini humo. Akisema

(SAUTI YA MARTIN GRIFFITHS)

“Kuna habari njema na habari mbaya. Habari njema ni kwamba suluhu ya kisiasa ya kukomesha vita hivi ipo na matakwa yake sio siri ni, kumaliza mapigano, kuondoa majeshi na kukabidhi silaha nzitonzito mahali husika kwa makubaliano ya kuanzishwa serikali ya mseto ambayo itazileta pande zote pamoja kwa muafaka wa ujenzi wa amani, haya yanawezekana.”

 

Image
Waathirika wa mizozo yemen. Picha: UNHCR

Na habari mbaya ni kwamba

 

(SAUTI YA MARTIN GRIFFITHS )

“Vita vimeongezeka na kutoa shinikizo kubwa katika hizi wiki chache.Idadi ya makombora ya masafa marefu yanayovurumishwa Saudia imeongezeka huku operesheni za kijeshi kwenye jimbo la Sa’ada zikishika kasi na kuleta athari mbaya,  mapigano na mashambulizi ya anga nayo yakiendelea katika sehemu mbalimbali Yemen yakiwemo majimbo ya Taiz, A1 Jawf, Ma'reb, A1-Hodeidah, Hajjah, A1-Baida na Lahj.”

Ameongeza kuwa watu wa Yemen wako katika taharuki na wanachohitaji ni ishara ya matumaini kwamba vita vitakoma hivi karibuni, kwa mfano kuhakikisha misaada ya kibinadamu inafika bila vikwazo na kuweza kufunguliwa kwa uwanja wa ndege wa Sana’a ili waweze kusafiri na kuungana tena na familia na jamaa zao.

Naye mratibu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura Mark Lowcock akihutubia mkutano huo kuhusu hali ya kibinadamu Yemen amesema

(SAUTI YA MARK LOWCOC)

zahma imeathiri familia na taasisi na sasa inaathiri karibu kila sekta na kila mfumo wa maisha Yemen,  lakini kwa hatua muafaka na za pamoja hali ya watu wa Yemen inaweza kuimarika.”

Watu takriban milioni 22 wanhitaji msaada wa kibinadamu haraka nchini humo na wengine msaada unashindwa kuwafikia kwa sababu za kiusalama na vikwazo hivyo ametoa wito

 

Mark lowcock , Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura, akihutubia baraza la usalama kuhusu hali ya yemen.
Picha na UN/ Mark Garten
Mark lowcock , Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura, akihutubia baraza la usalama kuhusu hali ya yemen.

(SAUTI YA MARK LOWCOCK )

”Pande zote katika mzozo ni lazima zichukuwe hatua madhubuti kuwalinda raia na kuwezesha fursa za kufikisha misaada ya kibinadamu kulingana na sheria za kimataifa za kibinadamu. Kumekuwa na hatua kiasi, ndege za misaada ya kibinadamu na meli vinasafiri hivyo ni vizuri, lakini bado tuna hofu na bidhaa za biashara kupitia bandari zote za Yemen hususan Hudaydah na Saleef. “

 

Amechagiza kutatua haraka hali hiyo kwani inachangia kwa kiasi kikubwa upungufu wa chakula na mahitaji mengine ya msingi. Amesema hatua zisipochukuliwa sasa  basi kuna hatari kubwa mlipuko wa kipindupindu ukarejea  hasa wakati huu msimu wa mvua ikiingia.