Watendeeni wema wahamiaji Yemen- UNHCR
Umoja wa Mataifa una wasiwasi mkubwa juu ya madhila yanayokumba wahamiaji, wasaka hifadhi na wakimbizi wapya nchini Yemen. Yaelezwa manusura hufyatuliwa risasi, hupigwa kila mara, hubakwa na hata huvuliwa nguo na kusalia uchi.
Wahamiaji, wakimbizi na wasaka hifadhi wapya wanaoingia wengi nchini Yemen kwa sasa wanakabiliwa na magumu kutokana na mgogoro unaoendelea huko ambao unasababisha mateso ya aina mbalimbali hasa kwa wageni wapya wanaowasili huko. Taarifa kamili na Assumpta Massoi.
Msemaji wa wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, William Spindler, amesema hayo leo akizungumza na waandishi habari mjini Geneva Uswisi.
Amesema wanaguswa na hali inayoendelea kuharibika hususan kwa wahamiaji, wakimbizi na wasaka hifadhi wapya nchini Yemen.
(Sauti ya William Spindler)
“Taarifa za unyanyasaji ndani mwa vituo vya kuwazuialia ni nyingi ambapo baadhi ya wageni wapya hunyanyaswa kingono. Manusura wameielezea UNHCR visa vya kufyatuliwa risasi, kupigwa kila mara, ubakaji wa watu wazima na watoto pamoja na udhalilishaji kama vile kuwavua nguo na kubaki uchi. Wakati mwingine hulazimishwa kushuhudia mauaji ya wenzao na pia kunyimwa chakula.”
Spindler amesema mgogoro unaoendelea nchini humo pamoja na hali ya kutokuwepo na usalama hutishia taasisi za dola na pia kudhoofisha utawala wa wa sheria.
Amesema hali hiyo imesababisha kuongezeka kwa visa vya kuwasafirisha kiharamu binadamu,kuwafukuza kutoka nchini humo na pia kudai pesa kutoka kwa wahamiaji. Ametaka wahusika kuwatendea mema wahamiaji.
Msemaji ameongeza kuwa kuanzia Februari mwaka huu, UNHCR imekuwa ikishughulikia hali ambapo wageni takriban 100 waliofika Yemen waliweza kukamatwa na kuwekwa ndani.
Walio kamatwa wanasema kuwa hutishiwa kurejeshwa walikotoka kwa nguvu pamoja na kunyanganywa mali zao na wanaowalangua au wakiwa vizuizini.