Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Boko Haram warejesheni watoto waliotekwa 2013 Nigeria:UNICEF

Picha: UM/Maktaba
Moja ya matembezi ya kushinikiza kuachiliwa kwa wasichana wa Chibok.

Boko Haram warejesheni watoto waliotekwa 2013 Nigeria:UNICEF

Haki za binadamu

Watoto zaidi ya 1000 waliotekwa Kaskazini Mashariki mwa Nigeria tangu 2013 bado hawajapatikana hadi leo na hii si haki limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF. 

Wito huo uliotolewa leo na UNICEF unajumuia wasichana 100 kati ya 276 wa shule ya sekondari ya Chibok waliotekwa mwaka 2014 na kundi la kigaidi la Boko Haram ambalo limeendelea kuwa mtihani mkubwa kwa raia, serikali ya Nigeria na jumuiya ya kimataifa.

UNICEF imeongeza kuwa miaka minne tangu kutekwa wasicha wa Chibok ikijongea ni kumbusho kwamba watoto Kaskazini Mashariki mwa Nigeria wanaendelea kuwa chini ya mashambulizi ya kiwango cha kutisha huku wakilengwa majumbani, mashuleni na hata katika maeneo ya umma.

Limesisitiza kuwa mashambulizi hayo hayakubaliki, ni ukatili na ni kuwapokonya watoto hao haki ya kuishi, kupata elimu na mustakhbali wao. Kwani watoto wana haki ya kusoma na kulindwa na madarani ni mahali ambapo wanapaswa kuhisi wako salama dhidi ya mashambulizi.

Tangu kuanza kwa mgogoro Nigeria waalimu 2295 wameuawa na shule zaidi ya 1,400 kusambaratishwa.