Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukata watesa watoto Korea Kaskazini

Mazao ya DPRK kama vile mpunga, mahindi, soybean na viazi yameharibiwa sana kufuatia ukame uliokithiri.
FAO/ Cristina Coslet
Mazao ya DPRK kama vile mpunga, mahindi, soybean na viazi yameharibiwa sana kufuatia ukame uliokithiri.

Ukata watesa watoto Korea Kaskazini

Msaada wa Kibinadamu

Lishe duni na kudumaa ni miongoni mwa mambo yanayokabili watoto nchini Korea Kaskazini kutokana na uhaba wa chakula.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA watoto hao ni miongoni mwa  watu milioni 10 sawa na asilimia 40 ya wananchi wote wa Korea Kaskazini ambao wanahitaji misaada ya kibinadamu ikiwemo chakula.

Hata hivyo ukata ni tatizo kwa mashirika yanayotoa misaada hiyo na ndio maana hii leo mashirika hayo yasema yatahitaji zaidi dola milioni 111 ili kusaidia mamilioni ya wananchi wa Korea Kaskazini ijulikanayo pia kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Korea au DPRK.

Mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa huko DPRK Tapan Mishra, amesema fedha hizo zitawezesha mashirika ya misaada kupatia wananchi chakula, huduma za kujisafi, huduma za afya kama vile chanjo na kusaidia wakulima kukabiliana na majanga ya asili.

Amesema misaada hiyo ya kibinadamu ni muhimu sana kwa wananchi wa Korea Kaskazini lakini upatikanaji wa fedha unasuasua akitolea mfano ombi la fedha la mwaka jana akisema hadi sasa ni chini  ya theluthi moja tu imepatikana.

Kwa mantiki hiyo Bwana Mishra amesema bila kupatikana kwa fedha hizo zilizoombwa, mashirika ya misaada hayataweza kutekeleza majukumu yao.