OPCW yathibitisha matumizi ya sumu ya kemikali Salisbury

12 Aprili 2018

Shirika la kudhibiti silaha za kemikali, OPCW limethibitisha matumizi ya kemikali ambayo Uingereza ilitaja kuwa imetumika kwenye tukio la tarehe 4 machi mwaka huu huko Salisbury, Uingereza. 

OPCW iliombwa na Uingereza kufanya uchunguzi huo ambao katika tukio hilo aliyekuwa jasusi wa Uingereza na Urusi Sergei Skripal na binti yake waliwekewa kemikali hiyo ya sumu.

Dkt. Ahmet Ahmet Üzümcü ambaye ni Mkurungezi Mkuu wa OPCW ameshukuru maabara ya chombo hicho iliyoteuliwa kuchunguza sampuli ya kemikali iliyotumiwa ili kubaini ukweli kuhusu matumizi ya kemikali hiyo.

Ujumbe wa Uingereza kwenye OPCW uliomba kuwa sekretarieti ya chombo hicho iwasilishe ripoti ya matokeo ya uchunguzi kwa nchi zote wanachama zilizotia saini mkataba wa kutokomeza silaha za kemikali, CWC na kuandaa ripoti fupi itakayochapishwa hadharani.

Sakata hilo la matumizi ya kemikali ya sumu dhidi ya jasusi hiyo na binti yake lilijadiliwa wiki iliyopita kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo wawakilishi wa Urusi na Uingereza walishutumiana juu ya suala hilo.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter