Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kunyonyesha watoto isiwe chaguo bali wajibu: WHO

Mama akinyonyesha mwanawe katika hospitali, Belgrade,Serbia.Picha/UNICEF/NYHQ2011-1166/Holt

Kunyonyesha watoto isiwe chaguo bali wajibu: WHO

Afya

Maziwa ya mama ni dawa kwa afya ya mtoto lakini pia ni mkakati mzuri wa kubana matumizi kwa familia na jamii hasa katika kupunguza gharama za matibabu , kwani kunaepusha maradhi. 

Hayo yamesisitizwa na shirika la afya ulimwenguni WHO na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, baada ya kutoa mwongozo wenye hatua 10 ambazo zikizingatiwa zitaokoa maisha ya watoto zaidi ya milioni 80 kila mwaka. 

Lakini pia kuna faida zingine lukuki za kunyonyesha kama anavyofafanua Dr Victor Aguayo mkurugenzi mwandamizi na mkuu wa mpango wa lishe wa kimataifa wa UNICEF

(SAUTI YA DR VICTOR AGUAYO)

“tunafahamu kwa hakika kwamba kunyonyesha kunalinda maisha, lakini pia kunasaidia ukuaji, na kuna ushahidi kwamba watoto ambao wamenyonyeshwa wanakuwa na uwezo mkubwa wa utambuzi wa mambo kuliko wasio nyonyeshwa, na kuna ongezeko la ushahidi kwamba watoto walionyonyeshwa wana wanaepuka kuwa na uzito wa kupindikia hapo baadaye ukilinganisha na wasionyonyeshwa, pia kwa wanawake wana hatari ndogo tu ya saratani kama za matiti na za mirija ya uzazi.”

Ameongeza kuwa unyonyeshaji watoto isiwe chaguo bali ni wajibu, lakini je watahakikisha vipi wajibu huo unatimizwa?

(SAUTI YA DR VICTOR AGUAYO)

Tutafikia azma hiyo kwa kuzisaidia serikali kuwa na sheria na será ambazo zitafanya kulinda suala la unyonyeshaji kuwa desturi na sio kitu cha kipekee au chaguo, na lazima liwe kitovu katika kuimarisha huduma za afya”