Tupambane ili utandawazi umnufaishe kila mmoja wetu

10 Aprili 2018

Dunia inajinasibu juu ya manufaa ya utandawazi duniani lakini Umoja wa Mataifa unaonya kuwa hatua zaidi zahitajika ili utandawazi uwe wa manufaa kwa watu wote.

Harakati za utandawazi haziwezi kurudi nyuma hivyo ni lazima kuchukua hatua kuhakikisha manufaa yake yanamfikia kila mtu.

Ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wakati akizungumza kwenye jukwaa la kila mwaka la Boao huko Hainan nchini China ambako yuko kwa ziara ya siku sita.

 

Mathalani ametaja manufaa ya utandawazi kuwa ni kuwanasua mamilioni ya watu kutoka katika lindi la umaskini na kwamba wengi wa watu wanaishi miaka mingi zaidi wakiwa na afya bora zaidi.

 

Kama hiyo haitoshi, utandawazi amesema umeunganisha   uchumi wa nchi duniani, biashara imepanuka bila kusahau maendeleo ya mawasiliano na teknolojia kuanzia Asia, Ulaya, Amerika hadi Afrika.

 

Hata hivyo amesema..

 

(Sauti ya Antonio Guterres) 

“Lakini tunapaswa kutambua kuwa idadi kubwa ya watu bado wanaachwa nyuma. Ukosefu wa usawa unakuwa kimfumo zaidi na unaongezeka. Mwelekeo wetu lazima uwe utandawazi ambao haumwachi nyuma mtu yeyote kama njia ya kuleta amani na maendeleo kwa watu, jamii na mataifa.”

 

Hata hivyo amesema 

 

(Sauti ya Antonio Guterres) 

“Lazima tuweke bayana. Utandawazi hautakuwa sawia kwa kutenga baadhi ya watu, vikwazo au kuengua wengine. Matatizo ya dunia yanahitaji suluhu za kimataifa. Mchango wa UN katika utandawazi sawia ni ajenda 2030 kwa ajili ya maendeleo endelevu.”

 

Jukwaa la Boao ni ushirikiano unaoleta pamoja viongozi wa serikali, biashara na wanataaluma kutoka bara la Asia na mabara mengine ili kubadilishana mawazo kuhusu maono yao ya masuala mazito yanayokabili ukanda wa Asia na kwingineko duniani.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter