Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

EYE kutokomeza homa ya manjano Afrika 2026

WHO na wadau wakutana nchini Nigeria kuzindua mkakati mpya wa kutokomeza homa ya manjano barani Afrika ifikapo mwaka 2026
Picha: WHO
WHO na wadau wakutana nchini Nigeria kuzindua mkakati mpya wa kutokomeza homa ya manjano barani Afrika ifikapo mwaka 2026

EYE kutokomeza homa ya manjano Afrika 2026

Afya

Sasa homa ya manjano imechosha bara la Afrika mkakati wa aina yake wazinduliwa huko Abuja, Nigeria.

Shirika la Afya ulimweguni WHO, leo limezindua mkakati wa kutokomeza homa ya manjano barani Afrika ifikapo mwaka 2026.

 

Mkakati huo ukipatiwa jina EYE au Eliminataion of Yellow ferev Epidemics, umezinduliwa leo huko Abuja, Nigeria katika mkutano wa siku tatu huku ikielezwa kwamba unalenga kufikia watu bilioni 1 kwenye nchi 27 zilizoathirika zaidi na homa ya manjano.

 

Malengo makuu matatu ya mkakati huo ni kuwakinga watu walio hatarini zaidi kuambukizwa homa ya manjano kwa kuwapatia chanjo kupitia kampeni mahususi, kuzuia kuenea ugonjwa huo katika nchi zingine, kudhibiti haraka milipuko na kuweka program za kawaida za utoaji wa chanjo.

 

Dkt. Tedros Ghebreyesus,ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa WHO amesema dunia iko hatarini kukumbwa na milipuko ya homa ya manjano na bara Afrika liko hatarini zaidi.

Amesema sindano moja tu inatosha kuepusha mtu kupata ugonjwa huo wa homa ya manjano.

 

Wakati wa mkutano huo wa siku tatu, wawakilishi kutoka WHO, shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, ubia wa chanjo duniani, GAVI wadau wengine na nchi za Afrika wataweka mpango wa kujumuisha mkakati huo katika ngazi ya kitaifa.

Hatua hii ni utekelezaji wa mkakati uliopitishwa na mawaziri wa afya wa nchi za Afrika mwezi Septemba mwaka 2017 wakati wa kikao cha 67 cha kamati ya kikanda ya WHO.

Uzoefu huko Afrika magharibi umedhihirisha kuwa mkakati huo wa EYE unaweza kufanya kazi pindi mlipuko wa homa ya manjano unaporipotiwa kwa kuwa nchi zinaweza kudhibiti kupitia kampeni kubwa za chanjo zilizojumuishwa na mipango ya kawaida ya utoaji wa chanjo.