Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwa mpinzani Libya ni tiketi ya mateso

Waandamanaji wa amani nchini Libya. Picha: UNHCR

Kuwa mpinzani Libya ni tiketi ya mateso

Amani na Usalama

Nchini Libya wanaume, wanawake na watoto wanakabiliwa na ukatili usio kifani kwa misingi ya makabila, misimamo yao ya kisiasa na hata kuwa na uhusiano na watu wanaodaiwa kuwa ni wapinzani. 

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo ikisema vitendo hivyo vinafanywa na makundi yaliyojihami yakiwemo yale yanayoungwa mkono na serikali na yale ya upinzani.

Watu hao wanashikiliwa korokoroni kinyume cha sheria na wanakuwa wanahusishwa na watu kama vile waandishi wa habari, madaktari, wanasiasa na wanaharakati ambao wanadaiwa  kuhusika kwenye mzozo wa kisiasa wa mwaka 2011. Wengine wanashikiliwa bila mashtaka kwa zaidi ya miaka 6 sasa.

Msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Elizabeth Throssell amesema makundi hayo yanapokamata watu hao yanadai malipo ya fedha kabla ya kuwaachilia huru.

Ofisi hiyo ya haki za binadamu inasema watu hao wanapaswa kuachiwa huru haraka na jamii ya kimataifa iingilie kati na zaidi yah apo.

(Sauti ya Elizabeth Throssell)

“Ripoti inatoa wito kwa mamlaka kulaani hadharani vitendo hivyo vya mateso, matendo maovu na mauaji kinyume cha sheria kwa wanaoshikiliwa. Halikadhalika ihakikshe uwajibikaji wa vitendo hivyo. Kushindwa kuchukua hatua hiyo siyo tu kutaongeza machungu kwa walioswekwa rumande na familia zao bali kutaongeza idadi ya vifo na kupeleka mrama mchakato wa ujenzi wa amani na maridhiano.”