Tujitathmini kabla ya kunyooshea vidole wahamiaji

9 Aprili 2018

Je wangapi kati yetu ndani ya familia zetu tuna historia ya uhamiaji zinazoimarisha urithi wa tamaduni zetu?

Ni swali la Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed wakati akifungua mkutano wa 51 wa kamisheni ya idadi ya watu na maendeleo hii leo jijini New York, Marekani.

Maudhui ya mkutano huo ni miji endelevu, hamahama ya watu na uhamiaji wa kimataifa ambapo BI. Mohammed amesema iwapo viongozi watatathmini familia zao na kutambua utajiri utokanao na muingiliano wa kimataduni, basi na hata uamuzi wao kuhusu hilo utakuwa na mantiki. Hivyo akawaeleza wajumbe wa mkutano kuwa anawatakia kila la kheri ili mkutano huo wa “Uweke mapendekezo ya kina, yanayotekelezeka kwa manufaa ya watu wanaohama, na pia kuwa na miji ambayo inakaribisha na kujumuisha wageni," amesema Bi. Mohammed.

Naibu Katibu Mkuu ametolea mfano mji wa São Paulo nchini Brazil ambao amesema awali ulisheheni matukio ya chuki dhidi ya wageni lakini tangu mwaka 2013 umekuwa ni mfano wa ukarimu kwa wageni kwa kuwa mji huo umetunga sera thabiti na mifumo ya kulinda kundi hilo. 

Amesema "Hatua hizi zimesaidia São Paulo kukaribisha na kukirimu jamii ya wahamiaji, na kusaidia wahamiaji na familia zao kupokea misaada bora na kulinda haki zao za kibinadamu.”

Mkutano huo ulioanza leo utamalizika Ijumaa wiki hii.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud