Asante China kwa kuendelea kutuunga mkono- Guterres

8 Aprili 2018

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres akutana na Rais Xi Jinping wa China mjini Beijing.

Umoja wa Mataifa unaendelea kutegemea uongozi wa China katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs,

Hiyo ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyotoa wakati wa mazungumzo yake na Rais Xi Jinping wa China mjini Beijing hii leo ambako yuko kwa ziara ya siku tano.

Guterres amesema mategemeo hayo ni kupitia ushirikiano wa kimataifa na pia mpango wa kimkakati wa ushirikiano kati ya nchi za Asia na Ulaya.

Halikadhalika wawili hao wamejadili pia suala la rasi ya Korea ambapo Bwana Guterres amepongeza China kwa  uchechemuzi wake kwenye kusaka suluhu ya kidiplomasia kwenye mzozo wa eneo hilo.

Katibu Mkuu wa UN António Guterres pia amekuwa na mazugnumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi mjini Beijing leo  Jumapili.
UN China/Zhao Yun
Katibu Mkuu wa UN António Guterres pia amekuwa na mazugnumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi mjini Beijing leo Jumapili.

Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu ameahidi utayari wa Umoja wa Mataifa wa kuendelea kuunga mkono mchakato wa dhati wa mazungumzo utakaowezesha kufanikisha aman endelevu na kuondokana na nyuklia kwenye rasi hiyo ya Korea.

Katibu Mkuu ametumia fursa hiyo pia kumpongeza Rais Xi kwa kuchaguliwa tena hivi karibuni kuongoza China na kuelezea shukrani zake kwa usaidizi wa China katika utekelezaji wa kazi za Umoja wa Mataifa.

Bwana Guterres amekuwa pia na mazungumzo na Waziri Mkuu Li Keqiang na Waziri wa Mambo ya Nje Wang Yi.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter