Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Burundi, twaheshimu mamlaka yenu lakini mwatutia wasiwasi

Wakimbizi wa Burundi waliokimbilia kusaka hifadhi nchini Rwanda kufuatia ghasia nchini mwao.
UNHCr/Anthony Karumba
Wakimbizi wa Burundi waliokimbilia kusaka hifadhi nchini Rwanda kufuatia ghasia nchini mwao.

Burundi, twaheshimu mamlaka yenu lakini mwatutia wasiwasi

Amani na Usalama

“Ni muhimu pande zote hususan serikali itangaze ahadi yake kwenye mchakato unaoongozwa na Jumuiya Afrika Mashariki, na kufikia makubaliano kabla ya uchaguzi mkuu mwaka 2020”

Bado hali ya kisiasa na kibinadamu nchini Burundi inatia wasiwasi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Taarifa ya rais wa Baraza hilo imesema kusuasua kwa mchakato wa mazungumzo baina ya warundi wenyewe na kitendo cha serikali ya Burundi kutojihusisha ipasavyo kwenye hatua hiyo kuwa ni miongoni mwa mambo yanayosababisha wawe na hofu juu ya mustakhbali wa kisiasa wa nchi hiyo.

Kwa mantiki hiyo Baraza kupitia taarifa hiyo linatoa wito kwa wadau wa Burundi kushiriki kwenye mchakato wa kusaka suluhu ya kisiasa bila masharti yoyote.

“Ni muhimu pande zote hususan serikali itangaze ahadi yake kwenye mchakato unaoongozwa na Jumuiya Afrika Mashariki, na kufikia makubaliano kabla ya uchaguzi mkuu mwaka 2020” imesema taarifa hiyo.

Wakimbizi wa Burundi wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto katika moja ya misafara yao ya kusubiri kwenye ufukwe wa ziwa Tanganyika ili wasafirishwe kwa boti kwenda kambi ya Nyarugusu mkoani Kigoma nchini Tanzania. Huduma sasa zinasuasua.
UNHCR/B. Loyseau
Wakimbizi wa Burundi wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto katika moja ya misafara yao ya kusubiri kwenye ufukwe wa ziwa Tanganyika ili wasafirishwe kwa boti kwenda kambi ya Nyarugusu mkoani Kigoma nchini Tanzania. Huduma sasa zinasuasua.

Ingawa hiyo Baraza la Usalama limesisitiza kutambua kwake mamlaka, uhuru wa kisiasa na kimpaka na Umoja wa Burundi.

Kuhusu hali ya kibinadamu, Baraza la Usalama limesema inazidi kudorora kila uchao, watu 180,000 wakisalia wakimbizi wa ndani huku 429, 000 wakisaka hifadhi nje ya nchi.

“Cha kusikitisha zaidi, baadhi ya wahisani wamesitisha misaada yao na hivyo tunasihi wahisani hao waangalie upya jinsi ya kurejesha ili kuokoa hali ya kibinadamu,” imesema taarifa hiyo.

Haki za binadamu pia zimeangaziwa, hususan kukamatwa watu kiholela bila kufunguliwa mashtaka, Burundi ikitakiwa kuchukua hatua kudhibiti hali hiyo.

Hata hivyo Baraza limekaribisha hatua ya tarehe 31 mwezi Disemba mwaka jana ambapo msamaha wa Rais uliwezesha kuachiliwa huru kwa baadhi ya wafungwa.

Image
Mama mkimbizi kutoka Burundi akiwa na watoto wake kambini nchini Tanzania. Picha: UNHCR