Miaka 50 baada ya kifo chake, wamkumbuka vipi Dkt. Martin Luther King Jr?

4 Aprili 2018

Unapomkumbuka Dkt. Martin Luther King Jr. fanya hivyo kwa kuendeleza mchango wake wa kutetea haki bila ghasia.

Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, maisha ya mwanaharakati na mtetezi wa haki za watu weusi nchini Marekani Martin Luther King Jr. yalifikishwa ukomo kwa mtutu wa bunduki.

Akimtambulisha kama gwiji wa maadili wa karne ya 20, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa alijitoa uhai wake akitetea usawa, haki na mabadiliko  ya kijamii bila ghasia.

Bwana Guterres anasema miongo mitano hata baada ya kifo chake, bado Martin Luther King Jr. ameendelea kuwa na ushawishi mkubwa kwa watu wengi kote ulimwenguni, hususan wale wanaosaka haki za binadamu, wanaobaguliwa na kukandamizwa.

Kama hiyo haitoshi, amesema harakati za hayati Martin Luther King Jr.za kupinga ubaguzi na kutetea haki za kijamii na utangamano, vina umuhimu zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote ule.

Na ni kwa kuzingatia hilo, Katibu Mkuu amesema Umoja wa Mataifa ulimtunuku hayati Dkt. Kingi tuzo ya chombo hicho kuhusu haki za binadamu mwaka 1978.

Kwa mantiki hiyo, Katibu Mkuu amesihi kila mtu amkumbukaye Dkt. King na mchango wake kwa haki duniani, afanye hivyo kwa kuendeleza mchango wa mwanaharakati huyo.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter