Kampeni ya mshikamano na wakimbizi yang’oa nanga

6 Aprili 2018

Siku ya kimataifa ya michezo kwa maendeleo na amani yaangaziwa huku kampeni maalum ikizinduliwa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi UNHCR leo limezindua rasmi ziara itakayofika kila kona ya dunia kuonyesha mshikamano na wakimbizi.

Shirika hilo linasema lengo kuu la ziara hiyo ni kuelimisha na kuchagiza umma kuchukua hatua kwa ajili ya watu waliolazimika kukimbia mizozo au mateso.

Ikipatiwa jina la kampeni ya #WithRefugees ziara  inaanzia kwenye kambi ya wakimbizi ya Za'atari nchini Jordan inayoahifadhi wakimbizi 79,000 kutoka syria, ikiambatana na michezo mbalimbali kwa ajili ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya michezo kwa ajili ya amani na maendeleo.

Kwa mujibu wa Leigh Foster mkuu wa kampeni, matukio na mabalozi wema wa UNHCR, kuchukua hatua kutawafanya watu kuonyesha mshikamano na kujali kwao kuhusu wakimbizi kwani kila hatua inayochukuliwa ni muhimu.

Matukio mengine yaliyopangwa katika ziara hiyo ya kimataifa ni pamoja na maonyesho ya mavazi yatakayofanyika Chicago yakijumuisha mavazi yatokanayo na vitambaa vilivyotengenezwa na wakimbizi nchi Kenya, mechi ya wakimbizi ya mpira wa miguu nchini Ireland, maonyesho ya picha mjini Paris, juma zima la matukio mbalimbali ya uelimishaji kisiwani Jeju korea Kusini na mashindano ya judo na tamasha nchini Afrika Kusini.

Na ziara itafunga pazia Oktoba Mosi kwenye sherehe za tuzo ya wakimbizi ya Nansen inayotolewa na UNHCR mjini Geneva Uswis.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter