Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hongera askari wetu kwa kuwazuia magaidi wa Al-Shabaab-AMISOM

Operesheni ya kukamata wafuasi wa Al Shabaab mjini Mogadishu nchini Somalia.(UM/Tobin Jones/maktaba)

Hongera askari wetu kwa kuwazuia magaidi wa Al-Shabaab-AMISOM

Amani na Usalama

Walinda amani wanne wameuawa na wengine sita kujeruhiwa  nchini Somalia mapema leo wakati askari wa kikosi cha kulinda amani cha muungano wa Afrika nchini Somalia -AMISOM- kilipokabiliana kijeshi na wapiganaji wa Al-Shabaab.

Taarifa iliyotolewa leo jumatatu na AMISOM  imesema kuwa vikosi vyao vilifanikiwa kuwarudisha nyuma magaidi wa Al -Shabab baada ya kushambulia  kambi tatu za vikosi vya AMISOM katika eneo la  Lower Shabelle.

Taarifa imemnukuu mjumbe maalum wa mwenyekiti wa tume ya Muungano wa Afrika kuhusu Somalia, balozi Francisco Caetano Madeira, akisifu jeshi la Muungano wa Afrika katika eneo la Lower Shabelle kwa kuonyesha ujasiri wao wakipambana dhidi ya magaidi wa Al Shabaab.

Taarifa imeongeza  kuwa Al Shabaab walihujumu mara kadhaa  kambi za jeshi zilizoko Quoryole, Bulomareer na Golwein na washambuliaji walipata cha mtema kuni.Katika mapigano hayo Al Shabaab takriban 30 wameuawa na magari manane yaliyowabeba yaliharibiwa pamoja na magari mawili yaliyokuwa yamejazwa  vilipuzi nayo yameharibiwa huku  silaha kadhaa zikikamatwa. 

Upande wa AMISOM ulipoteza askari wake wanne ilhali wengine sita wakijeruhiwa.