Tuhakikishe wanawake na wasichana wenye usonji hawaachwi na treni ya 2030: Guterres
Katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya uelimishaji kuhusu usonji, ambayo kila mwaka hua Aprili pili, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kusimamia haki ya watu wenye usonji na kupazia sauti ubaguzi dhidi yao.
Kupitia ujumbe wake mahsusi kwa siku hii siku Antonio Guterres amesema, kauli mbiu mwaka huu inatanabaisha umuhimu wa kuwawezesha wanawake na wasichana wenye usonji, kwani wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo vikwazo vya kupata fursa ya elimu na ajira sawia na watu wengine, wananyimwa haki zao za afya ya uzazi na haki ya kufanya maamuzi yao, lakini pia kutoshirikishwa katika utungaji wa sera za masuala yanayowahusu.
Guterres ameongeza kuwa kazi ya kupigania usawa na uwezeshaji wa wanawake lazima iwafikiwe wanawake na wasicha wote duniani ,na juhudi za kufikia malengo ya maendeleo endelevu lazima zizingatie ahadi ya ajenda ya mwaka 2030 ya treni hiyo kutomwacha yeyote nyuma.
Katibu Mkuu ametoa wito kwa kila mmoja katika siku hii kuongeza juhudi za kuchagiza ushiriki kikamilifu wa watu wenye usonji na kuhakikisha wanapata msaada wa lazima unaohitajika ili waweze kufurahia haki na uhuru wao wa msingi.