Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kengele ngapi zigongwe tudhibiti mabadiliko ya tabianchi? Guterres

Mabadiliko ya tabianchi yaathiri sekta ya uvuvi. Huyu ni vvuvi nchini Sudan. (Picha:World Bank/ Arne Hoel)

Kengele ngapi zigongwe tudhibiti mabadiliko ya tabianchi? Guterres

Tabianchi na mazingira

Mkutano na waandishi wa habari, Guterres amulika zaidi mabadiliko ya tabianchi na hatua anazoamini kuwa zinapaswa kuchukuliwa. Azungumzia pia matarajio yake kuhusu kinachoendelea rasi ya Korea na mvutano kati ya Urusi na mataifa mengine duniani.

Watu 900,00 barani Afrika wamekimbia makazi yao kutokana na ukame. Nchi za kusini mwa Asia zimeshuhudia mafuriko makubwa yaliyoathiri awtu milioni 41. Gharama za kiuchumi kutokana na majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi ni dola bilioni 320. Hii imevunja rekodi!

Ni takwimu baada ya takwimu, zikitolewa leo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini New  York, Marekani.

Bwana Guterres anasema..

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Mlolongo huu wa takwimu kama tsunami lazima uibue wasiwasi.”

Image
Mabadiliko ya tabianchi huenda sambamba na uhaba wa maji na wanaoathirika zaidi ni wanawake. (Picha:UNMISS)

Guterres amesema matumaini  yaliyoibuka baada ya kupitisha mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi, sasa yanafifia kutokana na kasi ndogo ya kudhibiti shughuli za kibinadamu zinazochangia madhara hayo.

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Naanza kuwa na wasiwasi kuwa ni kengele ngapi za tahadhari zinaapaswa kupigwa kabla dunia haijakabiliana na changamoto hizi.”

Katibu Mkuu amesema ni dhahiri shahiri kuwa ni vigumu kushughulikia matatizo ambayo yanaelezwa kuwa yatatokea miongo kadhaa ijayo licha ya kwamba athari za hali ya hewa tayari zinakabili dunia.

Image
Mafuriko yanayochangiwa na mabadiliko ya tabianchi. Picha: WMO

Bwana Guterres amesema zama za mawe hazikumalizika kwa sababu mawe yalimalizika duniani, la hasha! Bali amesema zama hizo zilimalizika kwa kuwa kulikuwepo na mbinu mbadala na bora zaidi.

Vivyo hivyo akisema matumizi ya nishati ya kisukuku lazima yapatiwe mbadala.

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Mabadiliko ya tabianchi yanakwenda kwa kasi kubwa kuliko kasi yetu ya hatua. Kile dunia inahitaji ni kuongeza kasi kwa kuwa na utashi wa kisiasa, ubunifu, uchangishaji fedha na ubia. Nasalia na kushawishika kuwa tuna uwezo wa kukabili  kilichotufika ili tuendelee kuwepo.”