Ujenzi mpya Iraq wapigwa jeki na WFP na Japan
Wakati serikali ya Iraq ikiibuka kutoka kwenye machafuko ya miaka minne, shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP ,limepokea dola milioni 10 kama mchango wa serikali ya Japan kusaidia ujenzi mpya Iraq.
Mchango huo utalisaidia shirika la WFP kuongeza shughuli za kuinua kipato na maisha ya Wairaq 9000 wasiojiweza. Na shughuli hizo zinalenga kufufua kilimo kupitia ukarabati wa mifereji ya mifumo wa umwagiliaji iliyoharibiwa kutokana na vita.
Fedha hizo pia zitatumia kutoa msaada wa chakula kwa muda wa miezi saba, kwa wakimbizi wa Syria 23,000 wanaoishi katika jimbo la Kurdistan nchini Iraq kupitia mpango wa vocha.
Kwa mujibu wa WFP mchango huo ni sehemu ya dola milioni 100 za fungu linalohitajika katika msaada wa kibinadamu kwa ajili ya wakimbizi wa ndani, watu wanaorejea makwao, wakimbizi walioenda nje na jamii zinazowahifadhi.
Tangu mwaka 2014 Japan imeshachangia dola milioni 60.3 kwa shughuli za usaidizi za WFP nchini Iraq.