Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Ethiopia wakabiliwa na mtihani Kenya:UNHCR

Balanish Tadese, mmoja  kati ya Waethiopia 10,000 wanaosaka hifadhi Moyale Kenya
UNHCR/Rose Ogola
Balanish Tadese, mmoja kati ya Waethiopia 10,000 wanaosaka hifadhi Moyale Kenya

Wakimbizi wa Ethiopia wakabiliwa na mtihani Kenya:UNHCR

Msaada wa Kibinadamu

Maelfu ya wakimbizi wa Ethiopia wanaohifadhiwa nchini Kenya hivi sasa wanakabiliwa na mtihani mkubwa wa kukidhi mahitaji yao ya msingi kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.  

Kambini nchini Kenya, nyanya wa miaka 55 amejawa na furaha furaha tele akibembeleza mjukuu wake Nuria, kichanga kilichozaliwa mara baada ya mama wa kichanga hicho kuwasili akikimbia machafuko Ethiopia.

Nyanya Darmigala Boru kutoka kabila la Borana ni miongoni mwa wakimbizi 10,000 walioingia Kenya tangu mwanzo wa mwezi huu. Kwa misukosuko waliyopitia nyanya huyo anasema hata haelewi bintiye Malicha doyo  aliwezaje kujifungua salama.

(SAUTI YA DARMIGALLMA BORU)

“Tulipokimbia nilikuwa naogopa , na hofu yangu kubwa ilikuwa binti yangu, alikuwa na ujauzito wa kujifungua wakati wowote, na hata nilishangaa aliwezaje kufika hapa.

Nyanya huyo alipotezana na bintiye Malicha Doyo njiani na kwa siku mbili akiwa na ujauzito wa miezi tisa alitembea bila kula wala kunywa maji na hakujua endapo ataonana tena  na mama yake. Lakini kwa bahati nzuri wamekutana tena kambini Kenya

Image
Wahamiaji kutoka Ethiopia. Picha ya IOM/T. Craig Murphy, 2016

(SAUTI YA MALICHA DOYO )

Sikujua kama nitafika, nilidhani nitajifungulia njiani, nilikuwa hoi na hakukuwa na kingine chcocote ambacho ningeweza kufanya, bnilihofia maisha yangu, hivyo nilitembea polepole hadi tukafika.

UNHCR inasema ingawa inashirikiana na serikali ya Kenya na wadau wengine kutoa msaada wa dharura kwa wakimbizi hao lakini kibarua ni kigumu , Dr. Burton Wagacha ni mratibu wa dharura wa UNHCR

(SAUTI YA DR BURTON WAGACHA)

“Changamoto iliyopo sasa ni chakula, wamewasili bila kitu chochote na wanahitaji vitu vya msingi kama vyombo vya kupikia , wanahitaji maji, wanahitaji malazi na wanahitaji huduma za afya”.

Ingawa jamii ya Halakano karibu na kambi hiyo imejitoa kimasomaso kuwasaidia wakimbizi wanaowasili hali bado ni ngumu.