Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukanda wa Sahel waona nyota ya jaha!

Wanawake nchini Chad wakichuuza mboga kwenye soko lisilo rasmi angalau kupata kipato cha kujikidhi maisha yao kwa kuwa mashambulizi ya Boko Haram na ukame vinakwamisha maisha  yao.
OCHA/Naomi Frerotte

Msaada wa Kibinadamu

Dola bilioni 2.7 kusaidia nchi za Sahel na kiwango hicho cha fedha kimetangazwa leo huko Mauritania na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J Mohamed  .

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J Mohammed ameelezea wazi azma ya  umoja huo ya kuunga mkono jitihada za kupiga vita ugaidi ulioshamiri kwenye ukanda wa Sahel.

Akihutubia mkutano wa ukanda huo huko Nouakchott, Mauritania, hii leo, Bi. Mohammed amesema Umoja wa Mataifa utafanya hivyo kwa kuzishirikisha nchi zote 10 zilizo kwenye ukanda huo ili hatimaye kuwe na amani ya kudumu.

Amesema licha ya ufinyu wa bajeti ya Umoja wa mataifa, Baraza la Usalama litaendelea kutoa kipaumbele katika jitihada za kutafuta suluhu ya amani ukanda wa Sahel kwa kuviwezesha vyombo vya usalama vya Umoja wa Mataifa kupata vitendea kazi vya kisasa ili kutoa huduma ya kulinda amani  kwa ukamilifu.

Ukosefu wa usalama na ukame vimesababisha njaa ukanda wa Sahel na kulazima mashirika ya Umoja wa Mataifa kama WFP kulazimika kugawa mlo kwa wakazi wa eneo hilo.
WFP/Sébastien Rieussec
Ukosefu wa usalama na ukame vimesababisha njaa ukanda wa Sahel na kulazima mashirika ya Umoja wa Mataifa kama WFP kulazimika kugawa mlo kwa wakazi wa eneo hilo.

Ili kukabiliana na changamoto za ukanda wa nchi za Sahel, Naibu Katibu Mkuu ametangaza kuwa Umoja wa mataifa na wadau wamechangia kiasi cha dola  bilioni 2.7 ili kusaidia mahitaji ya kibinadamu, usalama, elimu na mahitaji mengine huko Burkina Faso, Cameroun, Chad, Mali, Niger, Nigeria na Senegal.

Viongozi mbalimbali walihudhuria mkutano huo akiwemo rais wa Mauritania, Mohamed Ould Abdel Aziz   na Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika, Moussa Faki Mahammat.