Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Je tuko tayari kwa biashara mtandao? -Mukhisa

Mwelekeo sasa ni biashara mtandao lakini kwa umakini. (Picha:UNCTAD)

Je tuko tayari kwa biashara mtandao? -Mukhisa

Ukuaji wa Kiuchumi

Biashara mtandao inashika kasi, nchi zinazoendelea zina watumiaji wengi wa intaneti lakini bado hazinufaiki na biashara ya mtandaoni, kulikoni?

Biashara ya mtandao imekua duniani lakini bado wanufaika wengi ni nchi zilizojiandaa kuhimili kasi ya ukuji wa uchumi wa kidijitali.

Katibu Mkuu wa kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD, Dkt. Mukhisa Kituyi amesema hayo hii leo kwenye taarifa inatangaza kufanyika kwa wiki ya biashara ya mtandao duniani mwezi ujao huko Geneva, Uswisi.

Amesema mwaka 2016 kulikuwa na watu bilioni 1.4 walionunua bidhaa kwa njia ya mtandao, ambapo kiwango hicho ni ongezeko kwa asilimia 11 ikilinganishwa na mwaka 2015.

Thamani ya biashara hiyo ya mtandao ilikuwa ni dola trilioni 26 mwaka 2016 ambapo UNCTAD inasema Marekani ilishika usukani kwa kumiliki biashara yenye thamani ya dola trilioni 7.6.

Japan ni ya pili ikiwa kwa kuwa na asilimia 2.8 ya kiwango chote cha biashara ya mtandao jambo ambalo Dkt. Kituyi amesema linaonyesha kuwa bado nchi nyingi hazijajiandaa kunufaika na soko la biashara hiyo ya mtandaoni.

Mathalani amesema katika nusu muongo uliopita, takribani asilimia 90 ya watumiaji wapya wa mtandao wa intaneti ni wakazi wa nchi zinazoendelea, ambako serikali bado hazina sheria za kulinda faragha, hali ambayo itafanikisha biashara hiyo.

Amesema ni wazi kuwa uchumi wa kidijitali unaweza kuleta manufaa kwa nchi zinazoendelea lakini ni lazima kushughulkia masuala muhimu ili mfumo huo ulete mustakbali unaotakiwa.

Ni kwa mantiki hiyo, UNCTAD imeandaa wiki ya biashara mtandao mwezi ujao wa Aprili kuanzia tarehe 16 hadi 20 ili kuangazia ni kwa vipi mataifa  yanaweza kunufaika na biashara hiyo inayokua kila uchao.